Sunday, July 29, 2012

SIMBA SC WAJIPANGA UPYA

                                             WALAZIMISHWA KURUDI GYM


Kikosi cha simba 





MABINGWA wa Soka Tanzania Bara, Simba, wataingia kambini kesho kujiandaa na mashindano mbalimbali ikiwemo Ligi Kuu Bara inayotarajia kuanza mwishoni mwa mwezi ujao.
Msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema jijini Dar es salaam juzi kuwa uongozi wa Simba umechukua hatua hiyo baada ya kupata matokeo yasiyoridhisha katika Michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, ya Kagame iliyomalizika jana.

Simba iliishia robo fainali baada ya kufungwa mabao 3-1 na Azam FC katika mechi iliyokuwa na ushindani kwenye Uwanja wa Taifa.

Kamwaga alisema: "Uongozi umefikia hatua hiyo baada ya kuona wachezaji bado hawajawa  fiti hivyo wataendelea kufanya mazoezi ya gym kabla ya kurudi uwanjani...ile hali ilitutisha sana kwamba Simba ifikie hatua ya kuonekana haina uwezo."

Alisema kuwa kocha wa timu hiyo, Milovan Cirkovic ameondoka kwenda Serbia kwa mapumziko mafupi na anatarajia kurejea wiki chache zijazo.

Mbali na hayo Simba inajipanga na michuano ya BancABC inayotarajia kuanza Agosti 4 hadi 18 ambayo itashirikisha timu zilizoshika nafasi tatu za juu katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara na Ligi Kuu ya Zanzibar.

Nyingine ni timu iliyoshika nafasi ya kwanza kwenye Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara na Ligi Daraja la Kwanza ya Zanzibar ambazo nazo kwa kushika nafasi hizo zimeshaingia katika Ligi Kuu.